Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Kipolisi Mbagala limezuia mkutano wa hadhara wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo uliokuwa umepangwa kufanyika leo, Agosti 12, 2024. Uamuzi huu umesababisha sintofahamu na mjadala miongoni mwa wafuasi wa chama hicho na wananchi wa eneo hilo.
Akithibitisha taarifa hii, Naibu Katibu wa Habari na Uenezi wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo, amesema, “Ni kweli polisi wamezuia mkutano wetu wa Mbagala, na huu ni mwendelezo wa vikwazo ambavyo tumekutana navyo katika mikutano yetu ya hivi karibuni pasipokuwa na sababu za kueleweka.” Taarifa hii inaendelea kuibua maswali kuhusu sababu halisi ya kuzuiwa kwa mkutano huo.
Barua inayosambaa mtandaoni, ambayo inadaiwa kuandikwa na Kaimu Mkuu wa Polisi Mbagala, Robert M. John SP, inaonesha kuwa maombi ya ACT Wazalendo yalikataliwa, huku ikielezwa kwamba “Mikutano yote ya hadhara na ya ndani imezuiliwa hadi hapo yatakapotolewa maelekezo mengine.”
Jitihada za kutafuta maoni ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam zinaendelea, ili kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu uamuzi huu wa ghafla. Wafuasi wa ACT Wazalendo wamesema wataendelea kupigania haki yao ya kukutana na kuwasiliana na wananchi, licha ya vikwazo hivi vinavyowakabili.
#KonceptTvUpdates