Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umelaani kukamatwa kwa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ni Makamu Mwenyekiti Taifa Tundu Lissu, Katibu Mkuu John Mnyika, Mwenyekiti Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi, Wakili Deogratias Mahinyila, waandishi wa habari wa Jambo TV Ramadhan Khamis na Fadhil Kirundwa, wanaharakati na viongozi wa BAVICHA akiwemo Twaha Mwaipaya, Moza Ally, Deusdedith Soka na wengine wengi kwa idadi isiyo rasmi waliokuwa katika mchakato wa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani.
Taaarifa iliyotolewa na THRDC imeeleza kuwa inakadiriwa watu zaidi ya 300 wamekamatwa kwa tuhuma ambazo hazijawekwa wazi na Jeshi la Polisi Tanzania huku baadhi wakidaiwa kupigwa, hivyo kutoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuwaachilia huru bila masharti ili waweze kuadhimisha siku hiyo kama ambavyo vyama vingine tayari vimekwishaadhimisha pasina kukamatwa kwao.
“Deusdedith Soka na vijana wenzake wasiopungua 10 walikamatwa Agosti 10, 2024 majira ya saa mbili usiku wakiwa ndani ya ofisi za CHADEMA Wilaya ya Temeke na kupelekwa kwenye vituo mbalimbali vya Polisi ikiwamo Chang’ombe, Kilwa Road na Kigamboni kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali ndani ya ofisi ya chama chao”, imeeleza taarifa hiyo.
THRDC imeeleza kuwa katika nyakati tofauti tofauti mnamo Agosti 11, 2024 wanaharakati na vijana waliokuwa wakisafiri kwenda jijini Mbeya kwa ajili ya maadhimisho hayo walikamatwa ndani ya magari yao waliyokuwa wamekodi na kufanyiwa upekuzi katika maeneo ya Mikese, Morogoro, Iringa, Makambako na Mbeya.
THRDC imeeleza kuamini kuwa kukamatwa kwa watu hao wote kunalenga kuwazuia kufanya shughuli ya maadhimisho ya vijana duniani Agosti 12 jijini Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume cha Ibara ya 18 na 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa haki na uhuru wa watu kujumuika, kufanya mikutano, maadhimisho na kueleza mawazo yao.
“Haki hizi hazipo kwenye Katiba peke yake bali zipo kwenye Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia” Imeeleza taarifa hiyo.
THRDC imesema ukamatwaji wa watu hao unafifisha uhalisia wa maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekuwa akihubiri tangu alipoingia madarakani, kwani vijana wana haki ya kukusanyika na kuadhimisha siku yao, na kuwazuia kwa kuwakamata kunaweza kuhatarisha zaidi amani ya nchi kwa sababu wanaweza kutumia njia zingine kueleza hisia zao na kusababisha madhara makubwa.
“Tunatoa wito kwa viongozi wengine wa nchi kuanzia Rais wa Tanzania na wengine walione suala hili kuwa linatia doa nchi yetu hivyo wachukue hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwaagiza Polisi kuwaachia watu wote waliokamatwa ili waendelee na shughuli zao za maadhimisho ya vijana kama ilivyopangwa kama vile ambavyo Mhe. Rais amekuwa akisisitiza masuala ya demokrasia na 4Rs”, Imeeleza taarifa hiyo.