Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Mhe. Miraji Mtaturu, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa hatua yake ya kushirikisha wadau katika maboresho ya Kanuni za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) katika Sekta ya Madini. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa kikao cha mapendekezo ya maboresho ya kanuni hizo, Mhe. Mtatura alisisitiza umuhimu wa fedha za CSR kutolewa mapema mwanzoni mwa mwaka wa fedha ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi unafanyika kwa wakati.
“CSR inalenga kuboresha maisha ya mwananchi aliyepo karibu na mgodi. Natamani fedha ya CSR inapotoka tu mwanzoni mwa mwaka wa fedha ipelekwe Halmashauri ili iweze kutumika kutekeleza miradi kwa wakati,” alisema Mhe. Mtaturu.
Aliongeza kuwa maboresho ya kanuni hizo yanalenga kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi karibu na migodi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutoka kwenye shughuli za uchimbaji madini, na hivyo kuleta maendeleo katika maeneo yao.
Mhe. Mtaturu alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia kikamilifu katika kuboresha maisha ya wananchi na kuinua uchumi wa taifa.
#KonceptTvUpdates