Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Ummy Nderiananga, leo amepokea Jedwali la Uchambuzi wa Sheria Ndogo kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mhe. Ramadhan Suleimani Ramadhan. Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.
Katika hotuba yake wakati wa upokeaji wa jedwali hilo, Mhe. Nderiananga alieleza kuwa uchambuzi wa sheria ndogo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria zinazoandaliwa zinakidhi matakwa ya wananchi na zinatengenezwa kwa kuzingatia uhalisia wa mazingira ya nchi. Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya Bunge na serikali ni muhimu katika kuboresha mifumo ya kisheria nchini.
Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo walihudhuria kikao hicho, ambapo walijadili kwa kina uchambuzi uliofanywa na Kamati hiyo. Kamati ya Sheria Ndogo inawajibika kuhakikisha kwamba sheria ndogo zinazoandaliwa na kupitishwa na Bunge zinafuata taratibu sahihi na zinakubalika kisheria.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Ramadhan Suleiman Ramadhan, aliendesha kikao hicho na kuongoza mjadala wa uwasilishaji wa Jedwali la Uchambuzi. Mhe. Ramadhan alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa sheria ndogo zinaandaliwa kwa umakini ili zisiwe na mapungufu ya kisheria na kiutendaji.
Kupokea Jedwali la Uchambuzi wa Sheria Ndogo ni sehemu ya jitihada za serikali na Bunge kuboresha utungaji wa sheria ndogo ambazo zinaathiri moja kwa moja maisha ya wananchi wa Tanzania.
#KonceptTvUpdates