Tanzania imejiandaa kikamilifu kutumia fursa ya soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama wa Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPP) kwa kuunganisha miundombinu ya kusafirisha umeme na nchi wanachama wa umoja huo. Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, katika mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa EAPP uliofanyika nchini Uganda.
Dkt. Biteko amesema kuwa mkutano huo umekubaliana kuhusu masuala muhimu, ikiwemo kuridhia uwepo wa kitengo huru cha masoko kinachojitegemea, ambacho kitasimamia soko la pamoja la mauziano ya umeme kwa nchi wanachama. Tanzania imepanga kutumia umeme wa ziada unaotokana na Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kuuza umeme kwa nchi wanachama wa EAPP, huku pia ikinunua umeme wakati wa upungufu.
Kwa sasa, miundombinu muhimu inaendelea kuwekwa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili kuhakikisha kuwa Tanzania inajiandaa vyema kuingia katika soko hilo. Miongoni mwa miradi hiyo ni laini kubwa ya umeme inayounganisha Tanzania na Kenya kupitia Namanga, ambayo tayari imekamilika, na laini ya umeme inayounganisha Tanzania na Zambia (TAZA), ambayo itakamilika ifikapo mwaka 2026.
Mwenyekiti wa soko la pamoja la kuuziana umeme la nchi za Kaskazini Mashariki EAPP, Mhe. Dkt. Ruth Ssentamu, amesema kuwa hatua hizi ni sehemu ya juhudi za EAPP kuboresha uendeshaji wa shughuli zake kwa kushirikisha Makatibu Wakuu wa Nishati kutoka nchi wanachama katika muundo wa kiutawala wa EAPP.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, amesema kuwa uuzaji wa umeme katika soko hilo la pamoja utatoa fursa za ajira na kubadilishana wataalamu katika miradi ya kusafirisha umeme, hivyo kuongeza mapato ya TANESCO na kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
Mkutano huo uliofanyika Uganda ulihudhuriwa na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Dkt. Doto Biteko, pamoja na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
#KonceptTvUpdates