Waziri wa Kilimo, Hussein M Bashe, amekutana na Balozi Wiebe de Boer wa Ufalme wa Uholanzi kwa mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uholanzi katika sekta ya kilimo. Kikao hicho kilichofanyika mapema wiki hii kimeweka mkazo kwenye maendeleo endelevu kupitia miradi ya utafiti na uwekezaji.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Bashe alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miradi ya utafiti na maendeleo kupitia ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Aliweka wazi kuwa ushirikiano huu utasaidia kuboresha teknolojia na mbinu za kilimo nchini, hatua ambayo itawawezesha wakulima kuzalisha kwa tija zaidi.
Aidha, mazungumzo hayo yaligusia umuhimu wa kuchimba visima kwa ajili ya wakulima wadogo wa korosho. Waziri Bashe alieleza kuwa hatua hiyo itasaidia wakulima hao kufanya shughuli za kilimo mwaka mzima, badala ya kutegemea msimu wa mvua pekee. Aliongeza kuwa Bodi ya Korosho Tanzania ipo kuhakikisha maslahi ya wakulima na wanunuzi yanalindwa katika mnyororo wa thamani wa korosho.
Waziri Bashe pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wadau mbalimbali wa maendeleo wenye nia ya kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uholanzi unalenga kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa endelevu na yenye manufaa kwa wakulima wote nchini.
#KonceptTvUpdates