Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa USAID Maji safi ambao unatekeleza miradi ya maji hapa nchini kwa kushirikiana na Sekta ya Maji hivyo kusaidia kufikia malengo ya Serikali katika huduma ya maji.
Amesema hayo akifungua mkutano wa tathmini ya mwaka ya utekelezaji wa programu ya USAID Maji Safi ambayo itachangia katika kufika lengo la upatikanaji wa maji kwa asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95 kama ilivyopangwa na Serikali.
Amesema programu hiyo inatekelezwa katika wilaya 14 za mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Rukwa, Mwanza na Simiyu kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa kipindi cha miaka mitano.
Pamoja na kushiriki mkutano huo wa tathmini, Mhandisi Mwajuma ameshuhudia utiaji saidi wa ruzuku kati ya USAID Maji safi na Bonde la Rukwa na Nyasa kupata usaidizi wa kununua vifaa vya kisasa vya kupima msukumo wa maji katika mito makubwa.
“Mradi huu wa USAID Maji safi unatekelezwa katika maeneo ambayo bado uhitaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira ni mkubwa” Mhandisi Mwajuma amesema na kuongeza ni mfano mzuri ambapo serikali inashirikiana na wadau wake katika kufikisha huduma katika jamii.
Mwakilishi wa USAID nchini Tanzania Bi. Hiba Anwar amesema shirika hilo ni mdau mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania kwa miaka mingi na litaendelea kusaidia jamii ili ipate maendeleo endelevu.
Aidha, katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Mha. Mwajuma amezindua jina jipya la mradi huo ambapo awali uliitwa USAID Maji na Usafi wa Mazingira na hivi sasa mradi huo jina lake ni USAID Maji Safi (Clean Water and Sanitation) Project.
#KonceptTvUpdates