Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kufuatilia sakata la binti anayedaiwa kubakwa na kulawitiwa na vijana watano.
Kupitia mitandao yake ya kijamii, Dkt. Gwajima ameeleza kuwa amepokea maoni na maswali mengi kutoka kwa wananchi kuhusu tukio hilo, ambalo limezua mjadala mkubwa nchini.
“Ndugu wananchi, nimepokea maoni na maswali yenu kuhusu taarifa iliyotolewa na RPC wa Dodoma (SACP Theopista Mallya) kuhusu ‘Binti wa Yombo’. Nimewasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Yusuph Masauni, ambaye tayari analifanyia kazi suala hilo,” amesema Dkt. Gwajima.
Waziri huyo amesisitiza kuwa tukio hilo ni la kikatili na lisilo na utu, na kwamba binti huyo anastahili haki kamili. “Ni dhahiri kuwa alichofanyiwa ‘Binti wa Yombo’ ni kitu kibaya kisicho cha utu, na anastahili haki yake kwa mapana yote,” amesema.
Dkt. Gwajima amewataka wananchi kuwa na subira huku serikali ikifanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki, akihimiza kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa sheria. “Nawasihi tujipe muda na kuamini kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na itaonekana bayana,” alihitimisha Dkt. Gwajima.
#KonceptTvUpdates