Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limeeleza wasiwasi wake juu ya haki za jamii ya Wamaasai wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, wakisema kwamba kutowasikiliza ni kuwanyima haki zao za msingi.*
Kauli hii imetolewa kufuatia maandamano yaliyofanywa jana na mamia ya vijana na wanawake wa jamii ya Wamaasai, wakishinikiza Serikali kuwapatia huduma mbalimbali za kijamii ambazo wanahisi wanazinyimwa.
Akizungumza jana, Katibu wa TEC, Padri Charles Kitima, alisema, “Leo hii tunapozungumza ndugu zetu Wamasai wa kule Ngorongoro wanatuma ujumbe mbaya wenye taswira hasi kimataifa… unapowaeleza ni hiari yao kubaki Ngorongoro halafu ukiwanyima haki zao za msingi, huo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”
Maandamano hayo ya amani, ambayo yalidumu kwa takribani saa nne, yalisababisha kusimama kwa shughuli za utalii katika eneo hilo. Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania wamezitaka mamlaka za Tanzania kuheshimu haki za jamii hiyo kwa kusikiliza malalamiko yao na kuwapa mahitaji yao ya msingi.
Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2022, Serikali ya Tanzania imekuwa ikihamisha wakazi wa Ngorongoro kwenda Msomera, mkoani Tanga, kwa lengo la kupunguza msongamano katika eneo la hifadhi. Hadi sasa, takribani watu 7,000 wamehama kwa hiari, ingawa baadhi ya wakazi wameeleza kutokuwa tayari kuhama.
#KonceptTvUpdates