Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imeanza kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya Shilingi bilioni 184, ambao unalenga kumaliza changamoto za upatikanaji wa maji katika wilaya za Tarime na Rorya.
Mkurugenzi wa MUWASA, Nickas Mugisha, amesema kuwa tayari serikali imelipa Shilingi bilioni 20 kwa mkandarasi na utekelezaji wa mradi huo mkubwa umeanza rasmi. Mugisha alibainisha hayo wakati akikabidhi vifaa vya ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DP) katika kata ya Sabasaba, vitakavyosaidia wakazi wa mitaa ya Chomete, Nyangai, na Kimusi.
“Huu ni mradi wa muda mfupi ambao una tenki la maji lenye ukubwa wa lita 300,000 na pampu mbili zinazoweza kuzalisha lita 22,000 kwa saa moja. Mradi huu ni sehemu ya jitihada za muda mfupi, lakini tunao mradi mkubwa zaidi wenye gharama ya Shilingi bilioni 184 ambao ukikamilika utapeleka maji katika maeneo yote ya wilaya za Tarime na Rorya,” alisema Mugisha.
Viongozi wa mitaa ya Chomete, Nyangai, na Kimusi walipokea vifaa hivyo kwa furaha, wakishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuleta maendeleo katika maeneo yao. Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimusi, James Nyangai, alisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji ili viendelee kuwafaidi wananchi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi, akiwemo Abgael Zabron (47), wameelezea changamoto ya maji kukatika mara kwa mara na kupatikana mara mbili tu kwa wiki, wakitoa wito kwa serikali kutatua tatizo hilo haraka.
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Sabasaba, Charles, alitoa wito kwa viongozi wa mitaa kuhakikisha vifaa vya ujenzi wa vituo vya maji vinavyokabidhiwa havikai ofisini, bali vinatumika mara moja ili wananchi waanze kupata huduma hiyo muhimu.
#KonceptTvUpdates