Jeshi la Polisi limekanusha kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP Theopista Mallya, kuhusu tukio la binti aliyefanyiwa ukatili, na kusema kuwa kauli hiyo si msimamo wa jeshi hilo.
Kamanda Mallya, alipohojiwa na chombo cha habari kwa njia ya simu, alisema kuwa hata kama binti huyo alidaiwa kujiuza, hakustahili kutendewa ukatili huo. Kauli hiyo imeibua hisia kali na kusababisha malalamiko kutoka kwa umma.
Kutokana na hilo, Jeshi la Polisi limetoa taarifa rasmi likiomba radhi kwa yeyote aliyekasirishwa au kuguswa na kauli hiyo. Taarifa hiyo imeeleza kuwa ufuatiliaji unafanywa ili kupata ukweli wa tukio hilo, na kwamba hatua zaidi zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi.
Wakati uchunguzi ukiendelea, Mkuu wa Jeshi la Polisi amemhamisha Kamanda Mallya kutoka Dodoma na kumpeleka Makao Makuu ya Polisi mjini humo. Nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi. Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na uchunguzi wa kina ili haki itendeke katika suala hilo.
#KonceptTvUpdates