Jeshi la Polisi Tanzania, kupitia Kamishna wa Polisi Zanzibar, limetoa onyo kali kwa wanasiasa na viongozi wa vyama vya siasa wanaotoa matamshi yenye sura ya uchochezi, yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
Katika taarifa iliyotolewa kwa umma leo, Kamishna wa Polisi Zanzibar alieleza kuwa kumekuwa na ongezeko la matamshi ya uchochezi katika mikutano ya hadhara ya kisiasa. Alisema kwamba maneno ya baadhi ya wanasiasa yanakiuka faragha na heshima ya watu wengine, huku yakiwa na lengo la kuchochea chuki, dharau kwa mamlaka halali, na kuhatarisha amani ya jamii.
Kamishna alisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza ni haki muhimu katika demokrasia, lakini alionya kuwa haki hiyo inapaswa kutekelezwa kwa uwajibikaji mkubwa, bila kuathiri haki za wengine. “Uhuru wa kusema haujumuishi haki ya kushambulia faragha ya wapinzani wa kisiasa au mtu yeyote, wala matumizi ya lugha zenye chuki au kueneza habari za uongo,” alisema Kamishna.
Aidha, Kamishna alitoa wito kwa wananchi kukataa ushawishi au kutumiwa na viongozi wa kisiasa kwa madhumuni ya kuchochea vurugu. Aliwahimiza wananchi kutathmini kauli za viongozi wao na kuhamasisha mazungumzo ya amani badala ya vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kwa kuhitimisha, Kamishna wa Polisi Zanzibar aliwahakikishia wananchi kuwa jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kutumia uhuru wa kujieleza kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Taarifa hii imetolewa rasmi na Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, ikilenga kuhimiza utulivu na amani nchini huku ikitoa wito wa ushirikiano kati ya vyama vya siasa na Serikali katika kutafuta ufumbuzi wa amani kwa tofauti zao.
#KonceptTvUpdates