Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura amemhamisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, SACP Theopista Mallya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi SACP George Katabazi.
HABARI YAKE ALIYOTANGAZA YA MWISHO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Theopista Mallya amesema jalada la kesi ya vijana watano wanaotuhumiwa kutekeleza tukio la ubakaji na ulawiti wa binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam limekamilika.
Vijana hao wanaodaiwa kutumwa na afande, wanne kati ya sita wameshakamatwa ambao walipanga na kutekeleza uhalifu huo. Tukio hilo liliibua mijadala mikali maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni.
Ukamataji huo umewagusa pia watu wengine wanane, kati yao wakiwemo wanne waliokamatwa kwa kukiuka sheria na kusambaza picha mjongeo (video) za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, zilizoonyesha tukio hilo la ukatili.
Jana Jumapili, Agosti 18, 2024, RPC wa Dodoma, Theopista akizungumza juu ya kinachoendelea kuhusu watuhumiwa hao, alisema katika uchunguzi Jeshi la Polisi lilibaini vijana hao waliotuhumiwa kwa madai ya kutumwa, walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa.
“Kilichobainika vijana hao hawakutumwa na askari, walikuwa kama walevi na wavuta bangi tu, lakini yule dada alikuwa kama anajiuza ‘kahaba’.”
“Neno askari ni General (jumla) kwa kuwa hata mgambo ni askari, hivyo hatuwezi kulifafanua zaidi kwa kuwa haikubainishwa wazi na tunaliacha hivyo” alisema Kamanda huyo.