Klabu ya Young Africans imeweka wazi mipango na matarajio yao makubwa kuelekea mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital O, itakayochezwa Jumamosi hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kupitia ujumbe wake, msemaji wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisisitiza kuwa mashindano haya ya CAF yanatoa fursa ya kupeleka ujumbe mzito kwa wapinzani wao barani Afrika, hasa wale wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa. “Tutapeleka ujumbe ndani na nje ya uwanja. Msimu uliopita tulituma ujumbe kwa kujaza uwanja wa ugenini, na safari hii tuna matarajio ya kuujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Vital O,” alisema Kamwe.
Akizungumza kuhusu hamasa ya timu hiyo, Kamwe alieleza kuwa “Goli La Mama,” ambalo ni hamasa iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanza kutekelezwa kwa nguvu tangu mwanzo wa msimu. Alisema klabu hiyo imeanza kuangalia jinsi ya kufunga mabao mengi zaidi ili kupata fedha nyingi kutoka kwenye kampeni hiyo, kiasi cha kuweza kulipa mishahara ya wafanyakazi.
Kamwe pia alielezea furaha yao kwa kutokuwa na majeruhi katika kikosi, akisisitiza kuwa wachezaji wote wako fiti na wanaendelea na maandalizi ya mechi hiyo muhimu. “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu, mpaka sasa hatuna majeruhi katika kikosi chetu. Wachezaji wako fiti na tuko tayari kwa mchezo wetu wa Jumamosi,” aliongeza.
Msemaji huyo aliwahakikishia wanahabari na mashabiki wa Young Africans kuwa klabu hiyo ni kisima cha ubunifu, na kwamba wana mipango mingine mizuri zaidi ambayo itawapa nafasi ya kuandika historia nyingine kubwa kama walivyofanya hapo awali na matukio kama “Max Day” na “Pacome Day.” Hata hivyo, Kamwe alisisitiza kuwa mechi dhidi ya Vital O imepewa umuhimu wa kipekee kwa kuwa ni ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi hii inatarajiwa kuvutia umati mkubwa wa mashabiki, na Young Africans wana matumaini makubwa ya kuanza safari yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi mnono.
#KonceptTvUpdates