Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa ya kupinga amri ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali namba 673 la tarehe 02 Agosti, 2024 ambayo imewaondoa wananchi wote wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye ardhi yao kwa kufuta Kata, Vijiji na Vitongoji vyote vya Tarafa hiyo.
Taarifa ya CHADEMA iliyotolewa leo Jumanne tarehe 20 Agosti, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema imebainisha kuwa kabla ya amri hiyo, Serikali ilisitisha huduma za kijamii kwa wananchi hawa kama kuondoa huduma za Afya, elimu na kusimamisha miradi yote ya maendeleo kwenye Tarafa hiyo.
“Katika hali ya kuonyesha kuwa Serikali ilishafanya uamuzi huo ni kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhamisha taarifa za kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kutoka Ngorongoro na kuzipeleka Msomera Tanga bila ridhaa ya wananchi hao.” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha CHADEMA imesema inaungana na wananchi wa Ngorongoro na kuwa nao bega kwa bega hadi watakaporejeshwa kwenye ardhi yao ya asili huku ikilitaka Serikali ifanye yafuatayo; “
1. Serikali irudi mezani kuzungumza na wananchi hao ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
2. Serikali ifute amri hiyo kwani kuendelea kutumika kwa amri hiyo kutasabaisha maafa makubwa kwa wananchi wa Ngorongoro na kuhatarisha Amani ya nchi.
3. Tunaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi iheshimu Katiba ibara ya 74 na sheria ya Tume ya Uchaguzi ambazo zimeweka bayana kuwa Tume haitapokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote, hivyo irejeshe majina ya wapiga kura kwenye daftari la kudumu la wapiga kura walipojiandikisha kwa mujibu wa sheria.”
“Tutaendelea kushirikiana na mashirika na taasisi mbalimbali kuhakikisha kuwa wananchi wa Ngorongoro wanapata haki ya kuishi kwenye ardhi yao ya asili.” imesema.