Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameongoza majadiliano muhimu ya wananchi na viongozi wa mkoa huo, kwa ajili ya maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025-2050. Kikao hicho cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilifanyika tarehe 19 Agosti 2024, katika ukumbi wa uwekezaji, na kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wawakilishi wa wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Kanali Mtambi alieleza kuwa majadiliano haya ni sehemu ya mchakato wa kitaifa wa kukusanya maoni na mapendekezo kuhusu Dira mpya ya Maendeleo, ambayo itaanza kutekelezwa mwaka 2025. Aliweka wazi kuwa majadiliano haya yamefanyika tayari katika ngazi ya wilaya, na sasa yamefika ngazi ya mkoa kabla ya maoni hayo kupelekwa kwenye Tume ya Mipango kwa ajili ya hatua zaidi.
“Dira ya Maendeleo ya Taifa ni nyenzo muhimu katika kuongoza mwelekeo wa nchi kwenye masuala mbalimbali. Hivyo, mkoa wetu unayo nafasi ya kipekee ya kuhakikisha wananchi na viongozi wanashiriki kikamilifu katika majadiliano haya,” alisema Kanali Mtambi.
Mtambi alibainisha kuwa lengo la kikao hicho ni kutoa fursa kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Mara kutoa maoni yao juu ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, ambayo ipo katika hatua za awali za maandalizi. Aliendelea kusema kuwa Dira hiyo inaonesha matarajio na vipaumbele vya wananchi, serikali, na taasisi binafsi kwa muda mrefu, na mipango mbalimbali itawekwa ili kufanikisha malengo hayo.
Katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Jumanne Sagini, aliipongeza mkoa wa Mara kwa hatua kubwa zilizopigwa katika kuboresha miundombinu ya barabara. Alikumbusha kuwa hapo awali, wananchi wa Mara walilazimika kutumia njia za usafiri kupitia nchi za Kenya na Uganda wakati wa safari za kuelekea Dar es Salaam na mikoa mingine ya Tanzania. Sagini pia alisisitiza umuhimu wa kurejesha bandari ya Musoma ili iunganishwe na treni ya SGR inayotarajiwa kufika mkoa wa Mwanza, jambo ambalo litachochea maendeleo ya kiuchumi kwa mkoa wa Mara.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, alitoa wito kwa wataalamu wa mipango kuzingatia idadi ya watu itakayokuwepo mwaka 2050 wakati wa kutekeleza Dira hiyo. Prof. Muhongo alieleza kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na watu kati ya milioni 120 hadi 141 mwaka huo, hivyo mipango yote inapaswa kuakisi mahitaji ya watu wengi ili kuepuka kupangilia mipango kwa ajili ya watu wachache.
Aidha, Prof. Muhongo alitoa mfano wa mahitaji ya umeme, akisisitiza kuwa kwa sasa umeme unatosheleza kutokana na idadi ndogo ya watu, viwanda, na ofisi, lakini aliwataka wataalamu kuzingatia mahitaji halisi ya umeme kwa mwaka 2050 ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa uhakika.
Majadiliano haya ya Mkoa wa Mara ni hatua muhimu kuelekea katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050, na yanatarajiwa kuchangia katika kuhakikisha kuwa Tanzania inaingia kwenye awamu mpya ya maendeleo yenye msingi wa maoni ya wananchi na viongozi wake.
#KonceptTvUpdates