Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amepongeza hatua ya kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wa ubakaji na ulawiti wa binti mmoja maarufu kama “Binti wa Yombo,” ambaye kisa chake kilisambaa sana mitandaoni. Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Agosti 20, 2024, Mwabukusi ameweka wazi kwamba TLS haitakoma kwa hatua hiyo pekee, bali inataka pia yule aliyewatuma watuhumiwa kutekeleza kitendo hicho achukuliwe hatua za kisheria.
“Tunapongeza kufikishwa Mahakamani kwa wahalifu, lakini tunasisitiza kuwa mtu aliyesababisha kitendo kile kufanyika, ambaye ni mkosaji pia, naye afikishwe Mahakamani mara moja,” alisema Mwabukusi.
Kwa kuongeza, TLS imedhamiria kuhakikisha haki za binti huyo hazipotei. Mwabukusi alibainisha kuwa chama hicho kitahakikisha kesi hiyo inafuatiliwa kwa karibu kwa kumteua Wakili atakayekuwa akiangalia kwa karibu maendeleo ya shauri hilo.
“Tutaweka Wakili atakayekuwa akifuatilia kwa karibu kuona jinsi shauri hilo litakavyoendelea, na kuhakikisha haki za binti yule zinalindwa ipasavyo,” alisisitiza Mwabukusi.
#KonceptTvUpdates