Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) limeunda Kamati maalum itakayofuatilia jambo la Ngorongoro kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Idara, Wizara na Vyombo vyote vinavyohusika na suala la Ngorongoro ili kujua ukwell zaidi na kuhakikisha misingi ya sheria za Tanzania inafuatwa.
Akiongea DSM leo Aug 20,2024, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi amesema Kamati hiyo ambayo inatarajiwa kumaliza kazi ndani ya kipindi cha siku 30, inajumuisha Wajumbe Dr. Rugemeleza Nshala, Tike Mwambipile, Bumi Mwaisake, Laetitia Petro Ntagazwa na Paul Kisabo na miongoni mwa mambo mengine Kamati itafanya mashauriano na Taasisi mbalimbali pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro ili kujua uhalisia wa migogoro husika.
“Kamati pia itafanya mapitio ya Sera, Sheria na Mazoea na kuzichambua kuhusiana na umiliki wa ardhi kwa Wazawa pamoja na shughuli za uwekezaji na uhifadhi na kubaini uzingativu wa haki za msingi za Raia katika maeneo husika kwa kuzingatia Katiba, Sera na Sheria za Nchi, itaandaa kongamano (Symposium) la Kitaifa kuhusiana na namna bora ya kufanya mandeleo kwa kuzingatia na kulinda haki za Wazawa katika ardhi zao za asili pamoja na haki zao za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni katika maeneo yanayofikiwa na shughuli za uwekezaji”
“Kubaini mashauri au hatua zote ambazo zimechukuliwa na Walalamikaji pamoja na Walalamikiwa kisheria na kiutaratibu katika kuhakikisha uzingativu wa sheria kubaini majina ya Watu ambao kweli wameridhia kuondoka kwa hiyari kwenye maeneo yao na ambao hawakuridhia kuondoka kwa hiyari na walioamua kubaki katika eneo lao la asili Ngorongoro, kubaini na kulishauri Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika juu ya hatua zakuchua ili kupata ufumbuzi wa kudumu kuhusu swala la migogoro ya ardhi inayosababishwa na mipango ya uwekezaji au uhifadhi” imeeleza taarifa ya TLS.