Kamanda wa Kaunti ya Nairobi, Adamson Bunge, ametangaza kuwa wafungwa 13, akiwemo mshukiwa wa mauaji ya Kware, Collins Jumaisi, wametoroka kutoka Kituo cha Polisi cha Gigiri. Bunge alitoa taarifa hiyo lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu tukio hilo la kushtua.
Collins Jumaisi, ambaye amekuwa akihusishwa na sakata la miili iliyookotwa katika eneo la Kware, amekana kujihusisha na mauaji hayo, akidai kuwa aliteswa ili akubali mashtaka hayo. Hata hivyo, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imekanusha madai ya mateso na imeomba muda zaidi ili kuwatafuta mashahidi na familia za waathirika wa tukio hilo.
Sakata la miili kuokotwa Kware limezua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya wananchi wanadai kuwa miili hiyo ni ya waandamanaji waliouawa na polisi wakati wa maandamano ya kupinga Sheria ya Fedha (Reject Finance Bill). Wengine wanadai kuwa Collins Jumaisi anatumiwa kama kisingizio ili kuficha ukatili wa polisi.
Tukio la kutoroka kwa wafungwa hao linazua maswali mengi kuhusu usalama wa vituo vya polisi na linatilia shaka uadilifu wa uchunguzi unaofanywa kuhusiana na mauaji ya Kware. Serikali inatarajiwa kutoa taarifa zaidi ili kufafanua hali hiyo na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wafungwa waliotoroka wanakamatwa tena.
#KonceptTvUpdates