Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Mhe. OTHMAN ALI MAULID amewataka wananchi wa Nungwi kuacha tabia ya kusuluhisha kesi za udhalilishaji katika ngazi za familia na badala yake wazifikishe katika vyombo vya sheria ili zishughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Akizungumza na wananchi wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja katika utoaji wa elimu ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ukatili kwa watoto inayotolewa na Jumuiya ya Maendeleo ya Jamii na Huduma Zanzibar JUMAJAHUZA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, Mkuu huyo wa Wilaya amewasisitiza wananchi kutunza ushahidi ili kesi zifanikiwe Mahakamani.
Nae Wakili na Mwanasheria wa Jeshi la Polisi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi SADIK ALI SULTAN amewaasa wananchi kuacha tabia ya kudhalilishana kupitia mitandao ya kijamii kwani amesema kumekuwa kukijitokeza makosa ya udhalilishaji kupitia mitandao.
SHARIF KOMBO BAKARI na TUM HAJI JUMA wakaazi wa Nungwi wameviomba vyombo vya sheria kuzidisha bidii katika kukabiliana na matukio ya udhalilishaji ili kuyadhibiti Matukio hayo.
Jumuiya ya Maendeleo ya Jamii na Huduma Zanzibar JUMAJAHUZA imeamua kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu ya kupinga vitendo vya udhalilishaji katika maeneo mbalimbali ambapo Agosti 24 mwaka huu watatoa elimu kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja.