Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kuacha tabia ya kuwaficha na kuwanyima fursa muhimu ya kupata elimu.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kondoa mara baada ya kutembelea shule ya Msingi Iboni inayojumuisha watoto wenye mahitaji maalum akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani humo katika mkoa wa Dodoma.
Amesema licha ya serikali kujenga miundombinu ikiwemo mabweni na madarasa kwaajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum bado idadi ya watoto hao imeendelea kuwa ndogo katika vituo vya kutolea elimu.
Amesema mathalani katika Wilaya hiyo ya Kondoa, watoto 30 pekee wenye mahitaji maalum wamepelekwa katika shule ya Iboni ikiwa shule hiyo inauwezo wa kupokea wanafunzi 200.
Makamu wa Rais amesema kitaaluma watoto wenye mahitaji maalum wana uwezo mkubwa pamoja na vipaji. Amewahimiza viongozi wa serikali, dini, vyama na wananchi kutoa msisitizo wa kuwatafuta watoto wenye mahitaji maalum waliopo majumbani na kuhakikisha wanapelekwa kupata elimu.
Makamu wa Rais amekabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule hiyo ikiwemo magodoro, viti mwendo, vyakula pamoja na vinywaji. Shule ya Iboni inayojumuisha watoto wenye mahitaji maalum imekamilisha mradi wa Ujenzi wa Mabweni Mawilli ambao umegharimu shilingi milioni 270.9.
Mradi huo unatarajiwa kuondoa changamoto ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kusafiri umbali mrefu wa kutoka nyumbani kwenda shuleni. Mradi huo pia utapunguza changamoto ya wanafunzi kutokufika shule kwa wakati pamoja na kuchangia kuweka mazingira bora na salama kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.