Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutumia mamlaka yake kuunda Tume ya Mahakama ya Majaji ili kuchunguza tuhuma zinazohusu utekaji, upotezaji, na ukamataji holela wa raia nchini.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Mbowe alieleza kuwa inahitaji hatua za kisheria kali na za kina ili kukomesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu. “Tunamtaka Rais aunde kitu kinachoitwa Tume ya Mahakama ya Majaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi Mahususi ya mwaka 2019. Tume hii itachunguza tuhuma zote hizi za utekaji, upotezaji, na ukamataji holela wa raia,” alisema Mbowe.
Mbowe alisisitiza kuwa Tume hiyo inapaswa iwasikilize wahanga na mashuhuda, ifuatilie kwa karibu mamia ya Watanzania waliouawa katika hali ya kutatanisha, na kuchukua hatua stahiki. “Rais ana mamlaka haya, na Tume hii haiwezi kuundwa na mtu mwingine yeyote isipokuwa Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu. Kuliachia jeshi la polisi likakuachia taarifa eti hivi! Wanajiteka wenyewe! Ni huzuni,” aliongeza Mbowe kwa mshutumu.
Kiongozi huyo wa CHADEMA alikosoa hatua za hivi karibuni ambapo alidai kuwa taarifa zinazotolewa kuhusu matukio ya utekaji na ukamataji holela zinaonyesha hali ya kutokuwa na uwazi na uadilifu. Aliweka wazi kuwa chama chake kitaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo na kushinikiza hatua za haraka kutoka kwa viongozi wa serikali.
Mbowe pia alihimiza jamii na vyombo vya habari kuendelea kubaini ukweli na kuchangia katika kutatua changamoto hizi zinazohusiana na haki za binadamu na utawala bora nchini.
Taarifa zaidi zinatarajiwa baada ya utafiti wa kina na hatua zinazochukuliwa na mamlaka husika.
#KonceptTvUpdates