Msemaji wa timu ya Vital’O Fc, Arsene Bucuti amesema kuwa Klabu ya Yanga wanaweza kuzifunga timu kubwa za Uingereza ikiwemo Man United na Liverpool kutokana na ubora ambao kikosi cha Kocha Gamondi kilivyo kwa sasa.
Yanga Sc kwenye mchezo wao wa awali wa Michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika waliifunga Vital’O mabao 4-0 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na sasa watarudiana tena tarehe 24 Agosti,2024.
“Ukiangalia Yanga wanavyocheza unaona wanacheza vizuri na wanajua. Naweza kusema Yanga ni timu bora barani Afrika kwa sasa lakini mpira unabadilika. Yanga inaweza kumfunga hata Man United ama Liverpool lakini hawezi kuzifunga Arsenal na Man City.
“Timu kama Aston Villa, Everton… Yanga anaweza kuzipiga lakini kwa Vital’O hii Jumamosi ni kufa na kupona. Tunaomba tu ulinzi wa ule uwanja na wachezaji wao wasiingie uwanjani kwa mafungu wala wasipitie mlango wa nyuma, Yanga akinifunga pale kwa Mkapa nitakuwa shabiki wake. Yanga watapata aibu, tutawaaibisha.
“Mchezo wa kwanza walitufunga kwa sababu ya hali ya hewa, joto lilikuwa kali na upepo, sisi tunapindua meza, kitakuwa kisasi cha karne na tutawapiga Yanga kama nyoka,” amesema Baccuti.
“Yanga ilivyotufunga bao 4 nikakumbuka Yesu alivyotundikwa msalabani, lakini nikaona Yesu alifufuka siku ya tatu, na sisi tutafufukia kwenye Uwanja wa Mkapa pale. Sisi mambo tumeshamaliza, mabao matano tu.
“Kama Mlandege inaipiga Yanga kwa nini Vital’O isimpige Yanga, leo nakwenda Unguja kwa wazee wangu kuwauliza ni jinsi gani huwa wanaweza kuwafunga Yanga na Simba na Azam,” amesema Baccuti