Anaandika mwana mitandao maarufu Tanzania anayefahamika kama Ujugu Hapa
Nataka twende taratibu ili tuelewane. Mdogo mdogo mpaka mwisho. Kama unajijua una mihemko, usisome hili andiko, HALIKUHUSU!
Mimi nafahamu sehemu yenye furaha ukileta habari za huzuni watu lazima wakufikirie una vina saba vya uchawi. Kwa sasa Yanga ipo kileleni, kila mwaka inapata mafanikio ya kubeba vikombe, mashabiki wana furaha.
Inapotokea mtu anaisema Yanga kwa namna yoyote ile nje ya furaha waliyonayo, basi huyo mtu anaonekana kama Mchochezi, Mzandiki, na haitakii mema Yanga
Lakini mimi naelewa yote hayo, najitosa ili tukumbushane. Yanga kwa sasa ina furaha, ila ina matatizo na haijitambui. Kuna ‘Utoto mwingi’ unafanyika ndani ya Yanga
Ipo hivi, Tafsiri ya kutojitambua ni kwenda na mambo tofauti na vile inavyotakiwa. — NJE YA UTARATIBU.
Na ukifanya mambo tofauti na inavyotakiwa unakaribisha matatizo
Mimi najaribu kujiuliza je Yanga imekua ni klabu ya WAPARE?
Siongei kwa ubaya kuhusu wapare, ila inafahamika ni watu wanaopenda kesi sana. Sasa hizi kesi ambazo haziishi za Yanga kila msimu zinatokea wapi? Faida yake ni nini? Na anaesababisha ni nani, ili iweje?
Chini ya utawala wa Injinia Hersi, Kila msimu Yanga ina kesi za usajili, kati ya mchezaji na klabu ya Yanga ama Klabu ya Yanga na Klabu nyingine — Kesi kubwa huwa ni PESA ZA USAJILI
Tunarudi pale pale kuwa YANGA INA MATATIZO. Kwanini kila siku kesi ziwe kwao tu?
Naomba niwakumbushe;
> August 2023, Taarifa zilitoka Yanga ilikua na kesi na Gael Bigirimana. Yanga ilipigwa adhabu ya kutosajili mpaka imlipe mchezaji huyo pesa zake. Kesi hiyo ni mule mule tu kwenye matatizo ya pesa za usajili.
> April 12, 2024 Yanga ilifungiwa kufanya usajili kupitia kesi ya mchezaji ambae taarifa ya TFF haikutaka kumtaja jina. Yanga ilitakiwa ikamilishe malipo ya mchezaji huyo.
> April 30, 2024 – Yanga ilikua na kesi na Lazarous Kambole, Fifa wakaingilia kati, Yanga ikashindwa, na ikamlipa Kambole
> August 20, 2024 – Jana zimetoka taarifa Yanga ina kesi na Bechem United. Inatakiwa ilipe zaidi ya milioni 200 kutokana na kukiuka makubaliano wakati wanamsajili Okrah
> Yanga ilikua na kesi na Hafiz Konkoni. Kesi ya pesa za usajili. Nani hakumbuki hili?
> Yanga ilikua na kesi na Morrison, walivutana mashati sana, ila Yanga ikashindwa ile kesi
Hizi kesi zote, hakuna kesi hata moja ambayo Yanga ameshinda. Je hii inatupa picha gani?
> Moja, Inawezekana kitengo cha Sheria ndani ya Yanga ( Department of compliance) ina udhaifu, au inapungukiwa uzoefu wa kudeal na kesi za kimkataba za wachezaji
> Mbili, Inawezekana ndani ya Yanga kuna ‘Mtu’ anaichomesha Yanga kupata hizi kesi ili
‘Labda’ ajitengenezee mazingira ya kuipiga Yanga pesa
> Tatu, Inawezekana ndani ya Yanga usajili unafanywa kwa mihemko, na kupelekea kushindwa kufanya makubaliano vizuri ya kimkataba na wachezaji wanaosajiliwa
> Nne, Inawezekana Yanga inahitaji kuongezewa nguvu na wanasheria wenye uzoefu na mikataba ya wachezaji hasa wa kimataifa. Kwa kuwa ukiangalia kesi zote zilizotokea, hakuna kesi hata moja iliyomhusu mchezaji wa ndani ( Local Player)
> Tano, Juzi tu kulikua na kesi ya Magoma, inayoihusisha Yanga kupitia baraza la wadhamini. Nadhani ndio kesi pekee Yanga amepata ushindi, japo hisia zangu zinaniambia, huko mbeleni hii kesi itakuja kufufuka tena
Mtazamo wangu ni kuwa YANGA INA MATATIZO.
YANGA HAIJITAMBUI.
Laiti kama Yanga ingekua inajitambua, hizi kesi zisingekua zinajirudia.
Najua kwa sasa Yanga ina furaha, hakuna anaetaka kusikia hizi habari. Ila ipo siku isiyo na jina, kwa ninavyoijua Yanga na watu wake, watakuja kufukua haya makaburi ya hizi kesi
Sasa ni muhimu Yanga ijirekebishe kabla JUA HALIJAZAMA.
Ila kama hamtaki kunisikiliza, endeleeni kujificha kwenye kivuli cha furaha, na kuendekeza hizi kesi.
Bwana Yesu Asifiwe.
#UJUGUHAPA