Afisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe, amethibitisha kwamba mkataba wa nyota wao Clement Mzize utamalizika mwisho wa msimu huu wa 2024/25. Hata hivyo, Kamwe amekataa vikali taarifa zinazozungumzia kuondoka kwa Mzize, akisisitiza kuwa mchezaji huyo bado anabaki kuwa sehemu muhimu ya timu.
Katika taarifa yake, Kamwe alisema, “Mkataba wa Mzize unaisha mwisho wa msimu huu lakini nawahakikishia Clement Mzize bado yupo sana Yanga. Kama ndoto zenu ni Mzize aondoke Yanga kwa sababu ambazo hazina kichwa wala miguu, uongozi wetu hauwezi kuruhusu hilo jambo.” Kauli hii inatuma ujumbe wa wazi kwa mashabiki na wapenzi wa timu kuhusu msimamo wa klabu juu ya hatima ya mchezaji huyo.
Kamwe aliendelea kwa kusema, “Msimu huu tuna timu bora kuliko muda wowote ule, tunayo timu tishio sio tu ndani ya Tanzania hadi nje ya mipaka ya Tanzania.” Hii ni kauli ya kuonyesha kujiamini kwa timu na uwezo wake wa kushindana kwa kiwango cha juu, huku akipinga madai kwamba Mzize anahitaji kuondoka ili kuendelea kukua katika taaluma yake. “Nitashangaa kusikia watu wanasema Mzize inabidi atoke ili akakue zaidi, lakini watu hao hao hawaangalii tulipomtoa Mzize,” aliongeza Kamwe.
Afisa huyo alisisitiza kuwa klabu imejipanga vizuri, akisema, “Wananchi tupuuze maneno yao kwani lengo lao wanataka kutuvuruga.” Kamwe aliongeza kuwa Yanga ina nguvu ya ushawishi na kiuchumi inayowezesha kuendelea kuwa na wachezaji bora, akisisitiza kwamba klabu imekuwa na maendeleo makubwa katika kiwango cha Afrika.
Kwa upande mwingine, Kamwe alikemea vikali wale wanaoeneza taarifa zisizo za kweli kuhusu klabu, akisisitiza kuwa Yanga imekuwa klabu bora na kubwa barani Afrika. “Shida yenu hamuamini kama Yanga imekuwa klabu bora na kubwa AFRIKA,” alisema Kamwe, akituma ujumbe wa kuimarisha imani na msaada kwa timu.
#KonceptTvUpdates