Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza wanachama wa CCM kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwezi Januari mwakani ili kuwa na sifa ya kushiriki Uchaguzi Mkuu na kukihakikishia Chama Cha Mapinduzi ushindi wa kishindo kutokana na wingi wa wanachama wa CCM kupitia jumuiya zake.
Dkt. Mwinyi amesema hayo alipozungumza na Wajumbe wa Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu ya CCM ngazi ya Matawi, Wadi, Jimbo, Wilaya, na Mkoa katika viwanja vya Tibirinzi, Mkoa wa Kusini Pemba, tarehe 22 Agosti 2024.
Aidha, Dk. Mwinyi ameahidi kujibu kwa takwimu sahihi hoja zote zinazopotoshwa, hakuna jambo la kuficha na kwamba yanayosemwa na baadhi ya wanasiasa ni uzushi, chuki, na uongo.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kuwadharau wanasiasa wanaoleta sera za ubaguzi badala ya kueleza sera za maendeleo.
Vilevile, amesema kuwa Serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa kuvuka malengo katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, miundombinu, masoko, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, michezo, ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi wa Serikali na posho zao, pamoja na ongezeko la pensheni jamii kwa wazee na wastaafu.
Kwa upande mwingine, Wabunge na Wawakilishi wa Mkoa wa Kusini Pemba wamemchangia shilingi milioni moja Rais Dk. Mwinyi kwa ajili ya fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar mwaka 2025.