Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameagiza mkandarasi STECOL COMPANY kuongeza kasi katika ujenzi wa barabara ya Mianzini-Sambasha, inayounganisha barabara ya Mianzini-Ngaramtoni juu-Olemringaringa Sambasha, yenye urefu wa kilometa 18 katikati ya jiji la Arusha. Eng. Kasekenya alisisitiza kwamba kukamilika kwa barabara hizi kutasaidia kuboresha huduma ya usafiri na kuendeleza mvuto wa jiji maarufu kwa utalii nchini.
“Ongezeni kasi ya ujenzi, zingatieni ubora, wekeni taa na alama za usalama barabarani ili kuepusha ajali na kuwafanya watumia barabara kufurahia kuwa na barabara nzuri za lami na zinazopitika wakati wote,” alisema Eng. Kasekenya. Alisisitiza pia umuhimu wa wananchi kulinda alama za barabarani ili kuongoza madereva na watumiaji wa barabara kwa usalama.
Zaidi ya shilingi bilioni 22 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo. Katika ziara nyingine, Eng. Kasekenya alikagua barabara ya Usa River-Ngarenanyuki hadi Oldonyo Sambu, ambapo maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa lami yanaendelea. Alitoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha madaraja yanayojengwa yanakidhi viwango vya juu vya barabara ya lami.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Chilumba Mohamed, alihakikisha kuwa barabara zinazojengwa zitakidhi viwango vya juu vya ubora na hadhi ya jiji la Arusha. “Tutaendelea kutoa elimu ya matumizi bora ya barabara ili kuepusha ajali na kulifanya jiji la Arusha kuwa mahali salama pa kutalii na kuishi,” alisisitiza Eng. Mohamed.
#KonceptTvUpdates