Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kuanzisha kampeni mpya ya kitaifa inayolenga kuzuia ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto. Taarifa iliyotolewa kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii imesema kuwa kampeni hiyo, itakayobebwa na kauli mbiu “TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA,” inalenga kutoa elimu kwa watoto kuhusu masuala ya unyanyasaji na kuwajengea uelewa wa kujitambua.
Kampeni hiyo itawalenga zaidi watoto wa kidato cha kwanza, kidato cha tano, pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa vyuo. Jeshi la Polisi litatoa elimu maalum kwa walengwa hawa ili kuwasaidia kufahamu haki zao na kujitambua zaidi. Uzinduzi rasmi wa kampeni hii utafanyika mkoani Njombe, Agosti 29, 2024, na utaongozwa na Kamishna wa Polisi Jamii kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, CP Faustine Shilogile, huku Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, akiwa mgeni rasmi.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa kampeni hii itatekelezwa nchi nzima na Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha ulinzi wa watoto.
Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa na kuleta mabadiliko chanya kwa jamii ya Tanzania.
#KonceptTvUpdates