JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Kanda ya Ziwa, Elias Anania (20) kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu kupitia kundi sogozi la WhatsApp.
Inadaiwa mwanafunzi huyo amewataka wenzake kununua petroli na kuchoma askari polisi wenye sare popote watakakokutana nao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbroad Mutafungwa, alidai kuwa mbali na kuhamasisha askari kuchomwa moto, pia aliwataka wachome moto watumishi wa umma.
Alisema kijana huyo anadaiwa kusambaza ujumbe katika kundi hilo, akishawishi wenzake kununua petroli na vibiriti kushambulia askari wa jeshi hilo.