Jeshi la Polisi Tanzania limewakamata watu wanne zaidi katika sakata la mauaji ya Samwaja Sifael Said (22) mkazi wa Kijiji cha Chalunyangu mkoani Singida aliyeripotiwa kutoweka tangu Agosti 8, 2024 katika mazingira ya kutatanisha baada ya kwenda kuangalia mpira wa miguu na rafiki yake.
Katika taarifa mpya ya polisi iliyotolewa siku ya Jumatatu tarehe 26 Agosti, 2024 na msemaji wake DCP David Misime imeelezwa kuwa baada ya kukamatwa kwa watu watatu wa awali katika mkasa huo ambao ni Selemani Shabani Nyandalu ‘Hango’ (24) mkazi wa Chalunyangu, Saidi Haji Msanghaa ‘Mangu’ (24) mkazi wa kijiji cha Migungu na Kamba Kasubi (34) mganga wa kienyeji mkazi wa kijiji cha Migungu Mtinko, mapya mengine yaliibuka.
Polisi wameeleza kuwa waliongozana na wananchi na watuhuhumiwa hao hadi walikokuwa wamemfukia Samwaja Sifael Said baada ya kumuua, kukata sehemu zake za siri kisha kufukia mwili wake katika shimo na wakabaini mashimo mawili yakiwa na miili ya wanadamu.
“Agosti 24,2024 mashimo mawili yaliweza kubainika ambapo baada ya kufukuliwa ulipatikana mwili wa Gidion Samwel Mnyawi, miaka 53 mkazi wa Makuro ambaye mara ya mwisho alionekana amepakizwa kwenye pikipiki na watu wawili Oktoba 15, 2023 na taarifa za kutoweka kwake kuripotiwa Polisi”, ameeza Misime katika taarifa hiyo.
Aidha Polisi imesema mwili mwingine ambao haujatambuliwa na unahitaji mwendelezo wa uchunguzi wa wataalam wa kuchunguzi maiti na vinasaba (DNA) ilikuwa ni mabaki ya nyonga, paja la mguu wa kulia na kushoto.
“Mabaki ya miili ya watu hao wawili yamefanikiwa kubainika baada ya wananchi na askari kuoneshwa na Asha Bakari (51) mkazi wa Migugu ambaye ni mke wa Awadh Ramadhani ‘Wawa’ (54) ambao ni wakwe wa Nkamba Kasubi mganga wa kienyeji ambaye alikamatwa hapo awali”, taarifa ya polisi imeeleza.
Imeelezwa kuwa watu hao waliuawa na mkwe wake huyo akishirikiana na Selemani Shabani Nyandalu ‘Hango’ na Salum Awadhi ambaye bado anatafutwa.
Imedaiwa chanzo cha Gidion Samwel Mnyawi kuuawa ni kutokana na kitendo chake cha kuuza shamba mara mbili, ambapo aliwauzia Hawa Mohamed Sumwa (54) na Idd Hussein Idd (25) wakazi wa Makuro lakini baadaye ikabainika shamba hilo alishaliuza tena kwa mtu mwingine.