Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitaja sababu za kutaka simba aitwe jina la Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, mwenyewe amesema yupo sahihi kutokana na asili ya ukoo wao.
Rais Samia amesema aliamua hivyo kutokana na umachachari na ‘ukorofi’ wa mwanasiasa huyo. Rais Samia ametoa kauli hiyo mapema jana Agosti 25, 2024 alipokuwa akifunga Tamasha la Kizimkazi katika viwanja vya Mwehe, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
“Nataka niseme, kulikuwa kuna vijiclip vinarushwa, kulikuwa kuna simba machachari pale, mkorofi kidogo. Nikauliza, huyu simba mmempa jina? nikaambiwa bado, nikawaambia muiteni Tundu Lissu, mpeni jina lake huyu simba, kwa sababu alikuwa hatulii kama alivyo mwanangu Tundu Lissu,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Lissu alivyotafutwa na Mwananchi kuhusu jina lake kupewa Simba, amesema Rais Samia yupo sahihi kwani yeye amezaliwa kwenye ukoo wa mashujaa wa Kinyaturu, watu waliowahi kuua simba wala ng’ombe na wezi wa ng’ombe wao.
“Kwa Kinyaturu mashujaa hao huitwa ‘ahomi’ (umoja ‘muhomi’). Babu yangu mzaa baba, Mughwai, alikuwa muhomi; aliua simba aliyevamia na kuua ng’ombe wake.
Baba yangu aliyenizaa, Mzee Lissu naye alikuwa muhomi. Aliua simba mara mbili waliovamia na kuua ng’ombe wake,” amesema Lissu.