Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao ni wadhamini wakuu wa ligi kuu ya NBC Tanzania Bara, imeligusa Tamasha la Kizimkazi Zanzibar kwa kuandaa matukio ya michezo, burudani na utalii.
Miongoni mwa matukio iliyoandaa kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ni ‘Bongo and Zenji Flavour Night’ lililofanyika Paje, likimuhusisha pia Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tukio hilo limetanguliwa na mechi ya fainali ya ligi ya vijana wa Kizimkazi ijulikanayo kama “SAMIA KIZIMKAZI YOUTH CUP”, kwenye Dimba la New Amaan Complex, na kuongozwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.
Walioibuka na ubingwa wa ligi hiyo ni Shule ya Sekondari Kusini baada ya kuwafunga Shule ya Sekondari Muyuni mabao 3-0.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa utalii wa samaki aina ya kasa uliopo Pango la Salaam (Salaam Cave) , Rais Samia ameipongeza benki hiyo akisema “Kwa kuwa siku ya leo ni maalum kwa ajili ya NBC na TTCL, nitumie fursa hii kuwashukuru sana na kuwapongeza kwa jitihada zao katika kufanikisha tamasha hili tangu lilipoanzishwa”
Naye Mkurugenzi wa NBC, Theobald Sabi amesema wamekuwa na wana Kizimkazi tangu kuanzishwa kwake miaka tisa iliyopita malengo yao yakiwa ni kuigusa jamii kupitia michezo, utalii, burudani na kushiriki miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa.
“Benki ya NBC imejipanga kuweka mfumo maalum wa malipo ya kidijitali ili kurahisisha malipo ya watalii kwenye Pango la Salaam, na maeneo mengine kama haya hapa Zanzibar”, amesema Sabi.