Mwenyekiti wa kijiji cha Amani kilichopo katika Kata ya Mundindi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe Issa Luoga amenusurika kuuwawa wakati akipambana na mnyama Simba wakati wakimsaka baada ya kugundua ameingia kijijini hapo.
Akizungumza akiwa katika hospitali ya kanisa Katoliki iliyopo Kata ya jirani Lugarawa, mwenyekiti huyo amesema katika kumsaka Simba huyo walikuwa kundi kubwa lakini Kuna muda walidhani Simba kuelekea upande wa pili hivyo kundi hilo lilielekea upande huo huku yeye na mwenzake wakiwarudisha mbwa Ili waelekee upande huo ndipo ghafla akashtuka kuona Simba yuko nyuma yake.
Mkononi alikuwa ameshika bunduki aina ya gibole hivyo alifyatua risasi kumpiga na wakati akiandaa risasi ya pili alishtukia Simba tayari yuko mwilini ikambidi aanze kupambana na kwa mateke na ngumi huku mwenzake akiwa amepigwa na butwa Kisha akapata ujasiri na kwenda kuanza kumchoma mkuki Simba huyo huku akiuchomoa na kumchoma tena hatimaye akafanikiwa kumuua.
Aidha Simba huyo ameleta madhara katika mifugo ambapo ng’ombe wengi pamoja na mbuzi wameliwa na Simba huyo huku wamiliki wakiambulia mabaki kitu ambacho kimewapa hasira wananchi na kupelekea baada ya kuuwawa Simba huyo aligeuzwa kitowewo na kugawana nyama yake.