Mchezaji wa klabu ya Nacional ya Uruguay, Juan Izquierdo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 27.
Izquierdo alilazimika kuondoka kwenye mechi ya Ijumaa Agosti 23 dhidi ya Sao Paulo katika hatua ya 16 bora ya Copa Libertadores kwenye gari la wagonjwa baada ya kuanguka katikati ya mechi hiyo.
Mchezaji huyo alikimbizwa hospitali na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Albert Einstein mjini Sao Paulo.
Alibaki katika uangalizi maalum kwa kusaidiwa kupumua na usiku wa kuamkia leo Jumatano Agosti 28 klabu yake imetoa taarifa kuwa amefariki.
“Tunasikitika kutangaza kifo cha beki wa Uruguay, Juan Izquierdo kutokana na matatizo ya kiafya, salamu zetu pole kwa familia yake, marafiki na wafanyakazi wenzake katika timu. R.I.P.” ilisema taarifa ya klabu ya Nacional.
Juan Izquierdo ameacha mke aitwae Selena, binti mwenye umri wa miaka miwili na mtoto mdogo wenye umri wa siku 10.