Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeuondoa Uwanja wa Jamhuri uliopo Jijini Dodoma katika orodha ya viwanja vinavyotumika kwa Michezo ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2024/2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Agosti 27, 2024 na Bodi hiyo, imeeleza kuwa uwanja huo unaotumiwa na timu ya Dodoma Jiji umepoteza sifa zilizoainishwa kwenye Kanuni na Sheria za mpira wa miguu.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa eneo la kuchezea (pitch) la uwanja huo limeonekana kukosa ubora ambapo sehemu kubwa haina majani ya kutosha na yaliyopo ni dhaifu jambo linaloufanya uwanja huo kutokuwa salama kwa wachezaji.
Kufuatia mapungufu hayo, kikosi cha Dodoma Jiji kimetakiwa kutafuta uwanja mwingine watakao kuwa wakiutumia.
Sambamba na hayo Bodi ya ligi imevikumbusha vilabu vyote kuhakikisha vinaendelea kutunza miundombinu ya viwanja vyake katika kipindi chote cha msimu wa ligi kwani kushindwa kufanya hivyo kutashusha ubora wa viwanja hivyo na kusababisha viondolewe kwenye orodha ya viwanja vinavyotumika katika michezo ya ligi.