Mtangazaji maarufu wa kipindi cha “Jana na Leo” kinachorushwa na Wasafi FM, Edo Kumwembe, ametoa wito kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, kuacha kuzuia mijadala inayohusiana na watu kutoweka na kutekwa nchini.
Akizungumza katika kipindi hicho Alhamisi ya Agosti 29, 2024, Kumwembe alisema, “Spika Tulia (Dkt. Tulia Ackson) anapambana na ukweli, ukweli ni kwamba watu wanapotea, watu wanatekwa, hilo lipo. Kwa hiyo, asizuie hii mijadala ambayo Wabunge wanaihitaji. Sio suala la mihemko, kuna orodha ya watu ambao wametekwa au wametoweka katika mazingira ya kutatanisha.”
Kauli hiyo ya Kumwembe imekuja wakati ambapo kumekuwa na mijadala mikali kuhusu masuala ya utekaji na kutoweka kwa watu nchini Tanzania. Wito wake unaonekana kama shinikizo kwa viongozi wa Bunge kuruhusu mijadala ya wazi kuhusu suala hilo, ili kuleta uwazi na uwajibikaji kwa serikali na vyombo vya dola.
Mijadala ya watu kutekwa na kutoweka imekuwa ikiibua hisia kali miongoni mwa wananchi na viongozi mbalimbali, huku baadhi ya watu wakitoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama wa raia wote.
#KonceptTvUpdates