Wazazi na walezi wilayani Serengeti wameaswa kuacha kuingiza tamaa ya mali na kuzuia watoto wa kike kujiunga na vyuo vya ufundi stadi kwa ajili ya kuwaandaa kuolewa. Onyo hili limetolewa na Mkurugenzi wa ‘World Changer Vision Tanzania’, Sulus Samweli, wakati wa mahafali ya saba ya chuo hicho.
Katika hotuba yake, Sulus Samweli alibainisha kuwa bado kuna uwepo wa mila zilizopitwa na wakati wilayani Serengeti ambazo zinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu ya watoto wa kike. “Jamii inaendelea kuteseka kwa sababu ya mila hizi, na tunaiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya tabia hizi,” alisema.
Sulus alieleza kuwa kupitia chuo cha ‘World Changer Vision Tanzania’, wamekuwa na utaratibu wa kufuatilia familia zisizojiweza na kuchukua watoto wa kike kwa ajili ya kuwasomesha, lakini bado changamoto inabaki kuwa uelewa mdogo wa jamii inayowazunguka kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.
Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa asilimia 30 tu ya wanafunzi wa kike wanaoanza masomo ya elimu ya juu nchini Tanzania hufanikiwa kumaliza masomo yao kila mwaka. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2023, kati ya wanafunzi 100 wa kike wanaojiunga na vyuo vikuu, ni 30 tu wanaomaliza masomo yao kwa wakati. Hii inaashiria changamoto kubwa katika mfumo wa elimu wa Tanzania, hususan kwa watoto wa kike.
Baadhi ya mabinti wahitimu wa mahafali hayo walitoa wito kwa serikali kutunga sheria kali ambazo zitasaidia kukomesha vitendo vya baadhi ya wazazi na walezi kuwakatisha masomo na kuwapeleka watoto wa kike kuolewa.
Ester Magige, mmoja wa wahitimu wa chuo hicho, alisema, “Kuna baadhi ya wazazi wanakuja wanawakataza watoto wao kusoma na kwenda kufanyishwa kazi za ndani. Wakati mtoto angesoma, angepata kazi na hata huyo mzazi angenufaika na kazi hiyo, na huyu mtoto asingebaki kuwa tegemezi tena.”
Madai haya yanaonyesha wazi jinsi mila na desturi zilizopitwa na wakati zinaweza kuathiri ndoto na mustakabali wa watoto wa kike katika jamii. Inatarajiwa kuwa serikali itachukua hatua za haraka ili kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanapata nafasi sawa ya kupata elimu na kufikia malengo yao maishani.
#KonceptTvUpdates