Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Serikali imetenga shilingi Bilioni 31 ili kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo.
Amesema fedha hizo zitaiwezesha TARI kufanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu itakayowezesha kilimo cha kisasa kwa wakulima, kufanya ununuzi wa vifaa vya kisasa, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa maabara na watafiti ili kuwawezesha kubuni teknolojia zitakazosaidia kakabiliana na mabadiliko ya tabianchi hasa kwenye afya ya udongo na mbegu zitakazostahimili ukame, wadudu na magonjwa.
Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo kupitia TARI imeendelea kufanya uchunguzi wa changamoto zinazokabili uzalishaji wa mazao ya chalula na biashara hasa afya ya udongo, magonjwa na wadudu ili kubaini viashiria vya hatari kwa msimu husika na kutoa ushauri kwa wadau wa kilimo juu ya namna ya kukabiliana na vihatarishi hivyo.
Waziri Bashe ametoa kauli hiyo bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Neema Mwandabila aliyehoji kuhusu mkakati wa Serikali wa kufanya utafiti kwa mazao ya kilimo na biashara ili kubaini changamoto za msimu husika.