Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amethibitisha kwamba Serikali imelitambua deni la Shilingi Bilioni 1.52 linalotokana na mapunjo ya mafao kwa waliokuwa wafanyakazi wa Mgodi wa Kiwira Coal Mine na madeni ya Wazabuni kabla ya ubinafsishaji wa mgodi huo.
Dkt. Kiruswa aliyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kyela, Mhe. Ally Mlanghila Jumbe, aliyetaka kujua hali ya mchakato wa malipo ya madeni hayo. Alifafanua kuwa, baada ya uhakiki wa madeni hayo, tayari deni hilo limepelekwa katika Hazina ili lipwe pindi fedha zitakapopatikana.
“Mheshimiwa Spika, uhakiki uliofanywa ulibaini kuwa madeni ya wafanyakazi yalikuwa shilingi bilioni 1.024 kwa wafanyakazi 893 na madeni ya wazabuni, ikiwa ni pamoja na watoa huduma za ulinzi, yalikuwa shilingi milioni 496. Hivyo, jumla ya deni lote inafikia shilingi bilioni 1.52,” alisema Dkt. Kiruswa.
Dkt. Kiruswa alifafanua kwamba malalamiko kuhusu mapunjo ya mafao yalitolewa na Chama cha Wafanyakazi Mgodini (TAMICO), na Serikali ilifanya ukaguzi maalum kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mnamo Novemba 2008. Baadaye, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali alifanya uhakiki wa madeni hayo mnamo Agosti 2021.
Kulingana na taarifa za Wizara ya Madini, deni hili linatokana na changamoto zilizojitokeza katika utawala wa mgodi kabla ya ubinafsishaji, ambapo baadhi ya malipo yalicheleweshwa au kupunguzwa kinyume na taratibu. Serikali imeahidi kulipa madeni haya mara fedha zitakapotolewa, kuhakikisha haki inatendeka kwa wahusika wote.
#KonceptTvUpdates