Tamasha la “Tulia Cooking Festival,” ambalo lilifanyika jijini Mbeya tarehe 31 Agosti 2024, limefanikiwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Tamasha hilo lilijumuisha mashindano ya mapishi ya vyakula kwa kutumia nishati safi, likishirikisha mamalishe na babalishe 1,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.
Akihitimisha tamasha hilo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, aliwataka wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na nishati zisizo salama kama kuni na mkaa ili kulinda afya zao, kutunza mazingira, na kupunguza athari za kijamii na kiuchumi.
“Lengo la kuandaa tamasha hili ni kuongeza uhamasishaji kwa jamii kuhusu elimu na matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ajenda hii ni ya muhimu sana kwa taifa letu na imebebwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika na duniani,” alisema Dkt. Tulia Ackson.
Dkt. Tulia aliwapongeza mamalishe na babalishe walioshiriki katika tamasha hilo kwa kutumia jukwaa hilo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. Pia alizitaka taasisi mbalimbali nchini kuandaa matamasha kama hayo ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kusaidia katika kulinda afya na mazingira.
Aidha, Dkt. Tulia pia aliwapongeza wadau wa maendeleo, wakiwemo Kampuni ya gesi ya ORYX, Coca-Cola, EWURA, na wadau wengine kwa kudhamini Tamasha la Tulia Cooking Festival. Alisema kuwa mchango wao umewezesha elimu ya nishati safi ya kupikia kufikia wananchi wengi zaidi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, alibainisha kuwa Serikali imeandaa Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034. “Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni pamoja na kutoa mitungi ya gesi bure,” alisema Mhe. Kapinga.
Kwa sasa, takwimu zinaonyesha kuwa karibu asilimia 30 ya kaya za mijini nchini Tanzania zinatumia nishati safi kama gesi na umeme kwa ajili ya kupikia, ikilinganishwa na chini ya asilimia 10 kwa kaya za vijijini.
Takribani asilimia 85 ya kaya za vijijini na asilimia 60 ya kaya za mijini nchini Tanzania bado zinategemea kuni na mkaa kwa kupikia, nishati ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira na afya mbaya kwa watumiaji.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu 33,000 hufariki kila mwaka nchini Tanzania kutokana na magonjwa yanayohusiana na moshi wa majumbani unaotokana na kuni na mkaa. Zaidi ya hayo, matumizi ya nishati hizo yamechangia uharibifu mkubwa wa misitu, ambapo takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa takriban hekta 372,000 za misitu zinaharibiwa kila mwaka.
Kwa mwaka 2023, Serikali ya Tanzania ilitoa zaidi ya mitungi 104,000 ya gesi kwa kaya zenye kipato cha chini, na inatarajia kuongeza utoaji huu hadi mitungi 450,000 mwaka 2024, ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Kupitia Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Serikali inalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa hadi chini ya asilimia 40 ifikapo mwaka 2030 na kuongezeka kwa matumizi ya nishati safi hadi zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.
Mhe. Kapinga alieleza kuwa kuna aina nyingi za nishati safi za kupikia kama vile gesi, umeme, majiko banifu, na majiko mengine. Alisisitiza kuwa nishati safi ni bora zaidi kwa kuandaa chakula kuliko kuni na mkaa, ambazo zina madhara mengi kiafya na kimazingira.
Aidha, Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ubunifu katika sekta ya nishati safi ili kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa bei nafuu. “Serikali inaendelea na mikakati ya kuwasaidia watu wengi waweze kutumia nishati hii kwa gharama nafuu, na ninazisihi kampuni za gesi kuendelea kufanya ubunifu ili kuhakikisha wananchi wananunua gesi kwa kiasi cha fedha walichonacho,” alisema Kapinga.
Tamasha la Tulia Cooking Festival limeleta mwanga juu ya umuhimu wa nishati safi na jitihada za kuleta mabadiliko katika jamii. Wakati tukielekea kwenye uchumi wa kijani, matumizi ya nishati safi ni hatua muhimu kuelekea maendeleo endelevu. Kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, serikali inajitahidi kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata nafasi ya kutumia nishati safi kwa gharama nafuu, hivyo kuboresha afya zao na kulinda mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo
#KonceptTvUpdates