Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli na dizeli, kwa mwezi wa Septemba 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 04, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Mwainyekule bei za mafuta zimepungua kutokana na kushuka kwa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia, pamoja na kuboresha thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
Bei ya rejareja ya petroli inayochukuliwa Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kutoka Shilingi 3,231 kwa lita moja na kuwa 3,140, ya Bandari ya Tanga imekuwa Shilingi 3,141 kutoka 3,229, na ya Bandari ya Mtwara ni Shilingi 3,142 kutoka 3,304.
Bei ya rejareja ya dizeli ya Bandari ya Dar es Salaam imeshuka kutoka Shilingi 3,131 hadi 3,011 Septemba, Bandari ya Tanga imeshuka kutoka Shilingi 3,138 Agosti hadi Sh3,020, na ya Bandari ya Mtwara imeshuka kutoka Sh3,140 Agosti hadi Sh3,021 kwa lita.
EWURA imeeleza kuwa mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada za kupunguza gharama za maisha kwa Watanzania na kusaidia ukuaji wa uchumi.
Pia, imewahimiza wauzaji kufuata bei hizo mpya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa gharama nafuu.