Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Wizara ya Nishati kuendelea kuusimamia ipasavyo Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili ukamilike kwa wakati. Hayo yameelezwa leo Septemba 7, 2024, na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Kirumbe Ng’enda, wakati wa ziara ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo ambao utaingiza megawati 2,115 mara baada ya kukamilika.
“Wizara iendelee kusimamia kwa umakini mradi huu ili mashine zote tisa ziweze kukamilika kama ilivyopangwa,” amesema Mhe. Ng’enda.
Kamati hiyo imeipongeza Serikali kwa kuhakikisha mashine zilizosalia zinaendelea kukamilika na kufanya kazi, ambapo hadi sasa mashine tatu zimekamilika na zina uwezo wa kuzalisha megawati 705, huku mashine ya sita ikiwa kwenye hatua za mwisho kukamilishwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara ya Nishati imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na Kamati ya Bunge, ikizingatia ushauri na maelekezo yao. Mradi wa JNHPP umefikia asilimia 98 ya utekelezaji, huku mkandarasi akiwa ameshalipwa shilingi trilioni 6.3 kati ya trilioni 6.5 zinazotarajiwa.
Kapinga aliongeza kuwa Wizara itaendelea kusimamia mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, chini ya uongozi wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko.
#KonceptTvUpdates