Jeshi la Polisi Tanzania limeanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio la kutekwa kwa Ally Mohamed Kibao, Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), lililotokea usiku wa Septemba 6, 2024, eneo la Kibo, karibu na Tegeta. Kibao alikuwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga kwa kutumia basi la kampuni ya Tashrif wakati tukio hilo lilipotokea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David A. Misime, amesema kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa hiyo na kuanza uchunguzi mara moja ili kubaini kilichotokea, chanzo cha tukio hilo, na wale waliohusika.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amedai kuwa basi lililombeba Kibao lilizuiwa na magari mawili yasiyokuwa na alama zozote, na watu waliokuwa ndani ya magari hayo walikuwa na silaha. Watu hao walimchukua Kibao kwa nguvu. Mnyika ameishinikiza Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) kutoa maelezo kuhusu tukio hilo, akisema kwamba silaha zilizotumika ni za aina zinazotumiwa zaidi na TISS kuliko Jeshi la Polisi.
Hadi sasa, haijafahamika ni nani waliohusika na utekaji huo na nini kilichosababisha tukio hilo. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku viongozi wa CHADEMA wakitoa wito wa uwazi zaidi juu ya tukio hili.
#KonceptTvUpdates