Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezitaka Mamlaka za Udhibiti na Ununuzi wa Umma Afrika Mashariki kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji ili kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Jukwaa la 16 la Ununuzi wa Umma kwa nchi za Afrika Mashariki na uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) lililofanyika leo Arusha.
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali zinatambua kwamba fedha nyingi zinazotengwa kwenye bajeti kila mwaka zimekuwa zikitumika kupitia ununuzi wa umma. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imekuwa makini kuhakikisha kuwa fedha hizo kupitia ununuzi wa umma zinapata usimamizi makini.
Ambapo kupitia kifungu cha 7 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ya Mwaka 2023, Serikali imeipa Wizara ya Fedha jukumu la kuhakikisha inaandaa Sera ya Taifa na Mkakati wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ili kuhakikisha ununuzi na shughuli zote zilizofunganishwa katika mnyororo wa ugavi zinazofanyika kwenye taasisi za umma zinazingatia sera hiyo na mikakati itakayowekwa.
“ Naomba Waziri wa Fedha mlisimamie hili na haya ni maelekezo ya Mhe. Rais. Kupitia majukwaa yaliyofanyika yote yametilia mkazo maadili, weledi, uwazi na uwajibikaji na bila maadili wananchi hawezi kupata huduma, pia fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya wananchi kupata huduma zinaamriwa na kundi hili na kama hatuna taasisi imara za ugavi na ununuzi hatutapata matokeo ya fedha na hatimaye umasikini utaongezeka,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “Nawaomba mnapojadili leo mkumbushane umuhimu mkubwa wa kulinda taaluma yenu, ioneeni wivu isimamieni taaluma yenu akitokea mtu anafanya vitendo visivyofaa mkemeeni. Jisimamieni wenyewe, asitokee mtu katikakati ya manunuzi anataka kufanya vitendo visivyofaa, PPRA simamieni vizuri jambo hili ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.”
Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza mwaka 2001 kwa kutungwa kwa Sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma. Baada ya changamoto kadhaa, zilipelekea mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
“Serikali kupitia PPRA kama chombo cha Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ililenga kufanya mageuzi na kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma, kuhakikisha thamani ya fedha, uwazi, na uwajibikaji, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi na kujenga uwezo katika ununuzi na ugavi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amebainisha Dkt.Biteko.
#KonceptTvUpdates