WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watoa huduma za afya wa nchi wananchama wa kanda ya Afrika Mashariki kuondoa vikwazo vinavyozuia wagonjwa wanaotafuta matibabu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
“Hatua hii ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa uchumi wa kikanda na ukuaji wa utalii tiba.”
Ametoa wito huo (Ijumaa Agosti 30, 2024 ) alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Njerere (JNICC). Dar es Salaam
Amesema nchi wananchama ikiwemo Tanzania zimejitahidi kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya Kanda kwa matibabu.
“Kwa sasa ni wagonjwa wachache sana wanaosafiri nje ya nchi zetu kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa Sekta ya Afya kuwekeza nchini Tanzania.
Amesema Serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini.
“Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo, mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate teknolojia mpya na huduma za kibingwa.”