Kampuni ya Apple imezindua toleo jipya la iPhone huku ikiendelea kukabiliana na changamoto za kupungua kwa mauzo. Simu mpya ya iPhone 16, iliyozinduliwa rasmi Jumatatu, imekuja na kipengele kipya cha kitufe cha kamera kilichowekwa upande wa nje, hatua inayokusudia kuboresha matumizi ya kamera na kurahisisha upigaji wa picha. Mbali na kipengele hicho, Apple imesema simu hiyo imeundwa mahsusi kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba (AI), ikiwa ni jaribio la kuvutia wateja zaidi na kuimarisha wimbi la mauzo.
Mtendaji mkuu wa Apple, Tim Cook, alisema uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha uwezo wa simu za mkononi kufanya kazi zaidi kwa kutumia AI. “Simu hizi zitakuwa na uwezo wa kufanya mambo ambayo hapo awali yangechukua muda au yalikuwa nje ya uwezo wa simu za kawaida,” alisema Cook. Hata hivyo, Apple inakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa kampuni nyingine za teknolojia ambazo tayari zimeingiza vipengele vya AI kwenye simu zao. Hii imeweka shinikizo kwa kampuni hiyo kuboresha teknolojia zake ili kuwa mbele ya washindani wake.
Mauzo ya iPhone, ambayo huchangia karibu nusu ya mapato ya Apple, yamekwama katika miezi ya hivi karibuni. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mauzo hayo yalishuka kwa asilimia 1 katika kipindi cha miezi tisa hadi Juni 29, ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hii imeelezwa kuwa ni matokeo ya wateja kusubiri matoleo mapya au kutafuta simu zenye teknolojia bora zaidi kutoka kwa washindani wa Apple.
Apple imeweka matumaini makubwa kwenye iPhone 16, ambayo imekuja na betri inayodumu kwa muda mrefu, chipu zenye kasi zaidi, na vipengele vya faragha vilivyoimarishwa. Simu hiyo pia ni ya kwanza kutengenezwa mahsusi kwa kutumia teknolojia ya AI, ambayo Apple inaamini itawapa wateja wake sababu ya kuhamia kwenye toleo hilo jipya na kuimarisha mauzo yake ya siku za usoni.
#KonceptTvUpdates