Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Mhe. Ummy Mwalimu, tarehe 8 Septemba 2024 alifanya mkutano wa hadhara katika Kata ya Mwanzange, akielezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025. Akiongozana na Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Bakari Ali Mtavya, Mbunge Ummy alitoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa kuhakikisha ahadi za chama hicho zinatimizwa kwa wananchi wa kata na jimbo hilo.
Katika hotuba yake, Mhe. Ummy alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Tanga Mjini. Alisema kuwa Serikali imewekeza kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 429 kwa ajili ya kuboresha Bandari ya Tanga. Uboreshaji huo utaiwezesha bandari hiyo kupokea meli kubwa zaidi, ambazo tayari zimeanza kutia nanga.
Mbunge huyo alibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya jimbo hilo kwani itachochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya usafirishaji na biashara. “Miradi hii ya maendeleo si tu itaongeza nafasi za ajira kwa vijana wetu, bali pia itaongeza mapato ya Serikali na kuchochea ustawi wa kiuchumi,” alieleza Mhe. Ummy Mwalimu.
Aidha, aliendelea kuelezea mafanikio mengine katika sekta za elimu, afya, na miundombinu ambapo fedha nyingi zimeelekezwa kujenga na kukarabati miundombinu ya kijamii kama shule, zahanati, na barabara. Mhe. Bakari Ali Mtavya naye aliunga mkono hoja hizo, akisema kuwa Kata ya Mwanzange imepata manufaa makubwa kutokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionekana kufurahishwa na juhudi za Serikali, huku wakitoa shukrani kwa viongozi wao kwa kazi nzuri ya kusimamia maendeleo.
#KonceptTvUpdates