Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mbossa, mnamo Septemba 9, 2024, alikutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Meli la COSCO kutoka China, Bw. YangFan Chen, kujadili mbinu za kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya TPA na COSCO.
Katika mkutano huo, viongozi hao walijadili namna bora ya kuongeza ufanisi wa huduma za shehena zinazopitia bandari za Tanzania. Mazungumzo hayo yalilenga kuboresha huduma za uingizaji na utoaji wa mizigo ili kuhakikisha shughuli za bandari zinakwenda kwa kasi zaidi na kuwapa wateja huduma bora.
Bw. YangFan Chen, akiwa ameambatana na watendaji waandamizi wa COSCO, alitembelea maeneo mbalimbali ya huduma bandarini ili kujionea jinsi shughuli zinavyofanyika. Alieleza kuwa COSCO itaendelea kushirikiana na TPA kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata huduma kwa haraka zaidi, jambo litakaloimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China.
Mazungumzo haya yanatoa matumaini ya kuongezeka kwa ufanisi wa bandari za Tanzania, huku ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha biashara ya kimataifa kupitia usafirishaji wa majini.
#KonceptTvUpdates