Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, ametoa maagizo maalum kwa viongozi wa chama hicho, akisisitiza umuhimu wa uandikishaji wa wanachama kuanzia ngazi ya shina hadi taifa. Mongella alitoa maagizo haya alipomtembelea Balozi wa Shina namba 3, Safina Masanja Kitundu, katika tawi la Buduhe, Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Mongella amesema kuwa CCM ni chama chenye heshima na jukumu muhimu katika kulinda mustakabali wa nchi. Alisisitiza kuwa uandikishaji wa wanachama ni hatua muhimu katika kuhakikisha uimarishaji wa chama, na alihimiza viongozi kuhakikisha kuwa wanachama wa jumuiya za UWT, Wazazi, na Vijana wanandikishwa kwa ufanisi ili kuimarisha nguvu ya chama.
Katika hotuba yake, Mongella alibainisha kuwa mafanikio ya chama yanategemea kujikita kwenye ngazi za mashina na kufanya kazi kwa karibu na mabalozi wa shina. Alieleza kuwa mashina ndio msingi wa chama, hivyo ni muhimu kwa viongozi kufanya kazi kwa karibu na wanachama ili kuhakikisha uandikishaji unafanywa kwa usahihi na kwa kiwango kinachokubalika.
Ziara ya Mongella mkoani Shinyanga, inayotarajiwa kudumu kwa siku saba, inalenga kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2024 na kuimarisha uhai wa chama katika maeneo ya vijiji na mitaa. Mongella atakagua shughuli mbalimbali za chama na kutoa mwongozo juu ya jinsi ya kuboresha utendaji na kuimarisha mshikamano ndani ya chama.
#KonceptTvUpdates