Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, ameeleza kuwa alikaa kwa kipindi cha takribani miezi sita bila kulipwa chochote baada ya kukabidhi ofisi kwa CAG mwingine. Kipindi hicho kilianza mwezi Novemba 2019 hadi Mei 2020, ambapo alikumbwa na changamoto kubwa ya kutopewa malipo, jambo ambalo lilimlazimu kuandika barua kwa mamlaka husika kutafuta ufumbuzi.
Katika mahojiano na kituo cha redio cha @CrownMediaTz, Profesa Assad alisema: “Niliandika barua kwa Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) kwamba niko Dar es Salaam hapa na sijalipwa chochote hadi sasa, naomba mmalize haya mambo.” Hali hiyo ilimfanya kuwa na wasiwasi kuhusu haki zake za malipo baada ya kustaafu.
Profesa Assad alifafanua kuwa, baada ya muda, alipokea mafao ya kustaafu kwa hiyari, jambo ambalo alikataa na kusema kuwa hakustahi kwa hiyari bali aliondolewa kinyume na katiba. “Baadaye nililipwa mafao, wakati huo nilikuwa na miaka 58 na sikusaini chochote. Nikajiuliza nalipwaje mafao katika umri huo. Nikaomba nyaraka zilizonisababisha mimi nilipwe mafao haya, ndani ya nyaraka nikaona sababu ya kulipwa mafao ni voluntary retirement (kustaafu kwa hiyari),” alisisitiza Profesa Assad.
Amesema kuwa, hakuwa na makubaliano yoyote ya kustaafu kwa hiari na alishangaa kuona nyaraka zinaonyesha hivyo. Profesa Assad amesisitiza kuwa aliondolewa kinyume na taratibu za katiba na hivyo anadai haki zake kama zilivyowekwa na sheria.
#KonceptTvUpdates